Thursday, 27 October 2011

KATIBA YA UPENDO FOUNDATION

A:SURA YA KWANZA; UPENDO FOUNDATION
UPENDO FOUNDATION ni mpango ulioanzishwa mahususi wenye lengo la kujenga jumuiya/jamii ya watu wanaowasaidia kwa hali na mali watu wanaoishi katika mazingira magumu ya maisha, wakiwemo wanafunzi, yatima, wajane, wagane, wazee, walemavu, masikini na makundi mengine mbalimbali kwenye jamii yanayohitaji kusaidiwa kwa namna yoyote ile. Chama hiki hakifungamani na dini, kabila, vyama vya siasa au kanda yoyote ile. Mpango huu ulioanzishwa rasmi Februari 2011(huko Umbwe Sekondari).

B:SURA YA PILI; MAKAO MAKUU YA CHAMA
Makao makuu ya chama yatakuwa mkoani Arusha, S.L.P......

C:SURA YA TATU; MADHUMUNI/MALENGO
(i)Kusaidia makundi maalumu katika jamii nzima kama vile yatima, wajane, wagane, wazee, walemavu, wagonjwa, vijana, wanafunzi na watu wanaoishi katika mazingira magumu ikiwemo walio na UKIMWI.
(ii)Kutoa elimu kwa jamii juu ya umuhimu wa kusaidia watu wanaoishi katika mazingira magumu.
(iii)Kushirikiana na vikundi/watu mbalimbali wenye malengo ya kusaidia jamii ya watu wanaoishi katika hali ngumu ya maisha pasipo kujali itikadi zao za kisiasa au kidini.
(iv)Kuunda jamii ya watu wanaomjua na kumcha MUNGU katika Roho na kweli maana tunaamini jamii inayomcha na yenye hofu ya MUNGU hakika jamii hiyo huepukana na maovu mbalimbali.

D:SURA YA NNE; KUJIUNGA
(i)Aina ya uanachama ni wa kujiunga kwa hiari ya mtu mwenyewe.
(ii)Mtu yeyote anaweza kuwa mwanachama maadamu awe na akili timamu na kukubaliana na masharti ya chama.
(iii)Mwanachama atakuwa halali baada ya kufuata taratibu za kujiunga ikiwa ni pamoja na kujadiliwa na vikao husika na kuidhinishwa na yeye kukubali masharti ya chama.
(iv)Mwanachama atalazimika kutoa kiingilio cha tshs 10000 tu kwaajili ya kusajiliwa rasmi na kupatiwa kitambulisho, katiba na kadhalika.
(v)Kulipa ada na gharama zilizokubaliwa na chama mara baada ya kuidhinishwa kwa kipindi chote cha uhai wa chama.

E:SURA YA TANO; HAKI NA WAJIBU WA MWANACHAMA
(i)Haki ya kupiga kura na kupigiwa kura kwenye chama.
(ii)Kutoa mawazo na mapendekezo yenye kujenga umoja kwenye vikao halali vya chama.
(iii)Kuchangia michango iliyokubaliwa na chama na kuchangia katika muda unaostahili.
(iv)Haki ya kuhoji juu ya taarifa/matumizi ya fedha hali kadhalika na kuzijadili kwenye vikao halali vya chama.
(v)Haki ya mwanachama kujitoa/kujivua uanachama pindi aonapo madhumuni ya chama na taratibu zake zinakiukwa.
(vi)Mwanachama ana haki na wajibu wa kupanga na kutekeleza shughuli mbalimbali za chama katika mkoa aliopo.

F:SURA YA SITA;UONGOZI,KAZI ZA VIONGOZI NA UCHAGUZI

1)SEKRETARIETI YA KUDUMU
Chama kitakuwa na sekretarieti ya kudumu ambayo itaundwa na waasisi watano wa chama hiki, ambao watakuwa na nafasi ya mwenyekiti, makamu mwenyekiti, katibu, katibu msaidizi na mhasibu.
1.1)KAZI ZA VIONGOZI
(i)MWENYEKITI
-Ataongoza mikutano yote ya chama na sekretarieti kama atakavyo itisha.
-Atasimamia uimarishaji wa shughuli zote za chama.
-Atakuwa muangalizi mkuu wa shughuli zote za chama.
-Atakuwa na uamuzi wa mwisho kwenye mikutano ya chama na vikao vya sekretarieti.
-Atakuwa na mamlaka ya kuunda ama kufuta kamati mbalimbali baada ya kushauriana na sekretarieti.
(ii)MAKAMU MWENYEKITI
-Atakuwa msaidizi mkuu wa mwenyekiti.
-Atafanya shughuli zote atakazopewa au kuelekezwa na mwenyekiti.
-Atafanya shughuli zote za mwenyekiti akiwa hayupo.
(iii)KATIBU MKUU
-Atakuwa msemaji na mtendaji mkuu wa shughuli zote za chama.
-Atatunza kumbukumbu zote na mali za chama.
-Atahakiki na kuratibu mikutano yote ya chama.
-Atafanya shughuli zote kama atakavyoagizwa na mwenyekiti.
(iv)KATIBU MSAIDIZI
-Atakuwa msaidizi mkuu wa katibu mkuu.
-Atafanya shughuli zote atkazoagizwa na viongozi.
-Atafanya shughuli zote za katibu mkuu atakapokuwa hayupo.
-Atasaidiana na mhasibu pindi atakapoombwa na mhasibu au viongozi wake.
(v)MHASIBU
-Atapokea na kupeleka benki michango yote ya chama na mapato kutoka vyanzo mbalimbali.
-Atawajibika kufanya malipo yote ya wanachama kama atakavyoelekezwa na mtendaji mkuu wa chama(katibu mkuu) baada ya kuidhinishwa na chama.
-Atawajibika kutoa taarifa ya mapato na matumizi kila baada ya miezi sita.
(vi)MLEZI
Chama kitakuwa na mlezi ambaye atateuliwa na sekretarieti ya kudumu, kazi zake zitakuwa kama ifuatavyo:-
(i)Atakuwa na nafasi ya kuhudhuria baadhi ya vikao vya sekretarieti ya kudumu na chama.
(ii)Atakuwa mshauri wa masuala mbalimbali kwenye chama na sekretarieti ya kudumu.
(iii)Atakuwa na wajibu wa kuunganisha na kutangaza chama kwa watu,taasisi na sehemu mbalimbali ndani na nje ya nchi kwa manufaa ya chama.

2)KAMATI YA NIDHAMU
Kamati hii itaongozwa na wajumbe watano ambao watashughulikia mambo mbalimbali yahusuyo nidhamu za wanachama na viongozi na kutoa mapendekezo kwa sekretarieti ya kudumu. Kazi zake ni kama ifuatavyo;
-Kufuatilia utekelezaji mzuri wa katiba.
-Kuwajadili na kuwaonya wanachama na viongozi pindi wanapokosa nidhamu.
-Kufanya kazi watakazopewa na sekretarieti ya kudumu ikiwemo kufanyia uchunguzi tuhuma mbalimbali kama vile ubadhirifu.
-Kutoa mapendekezo kwa sekretarieti ya kudumu yenye lengo la kuimarisha umoja, mshikamano na maendeleo ya chama.

3)UONGOZI WA MKOA
Kila mkoa utakuwa na viongozi watatu ambao ni mwenyekiti, katibu na mhasibu (wasaidizi wakihitajika mkoa utapendekeza kwa sekretarieti ili kutoa idhini.
3.1)KAZI ZA VIONGOZI WA MKOA
(i)MWENYEKITI
-Ataongoza mikutano yote ya chama na viongozi kama atakavyoitisha.
-Atasimamia uimarishaji wa shughuli zote za chama.
-Atakuwa muangalizi mkuu wa mali za chama.
-Atakuwa na uamuzi wa mwisho kwenyee mikutano ya chama na vikao vya viongozi.
-Atapokea na kutekeleza mambo/shughuli mbalimbali atakazoelekezwa na sekretarieti ya kudumu.
(ii)KATIBU MKUU
-Atakuwa msemaji na mtendaji mkuu wa shughuli zote za chama.
-Atatunza kumbukumbu zote na mali za chama.
-Atahakiki na kuratibu mikutano yote ya chama.
-Atafanya shughuli zote kama atakavyoagizwa na mwenyekiti/viongozi wake.
(iii)MHASIBU
-Atapokea na kupeleka benki michango yote ya chama na mapato kutoka vyanzo mbalimbali.
-Atawajibika kufanya malipo yote ya wanachama kama atakavyoelekezwa na mtendaji mkuu wa chama(katibu mkuu) baada ya kuidhinishwa na chma.
-Atawajibika kutoa taarifa ya mapato na matumizi kila baada ya miezi sita.

4)UCHAGUZI
Uchaguzi utafanyika kila baada ya miaka mitatu katika kila mkoa ambapo sekretarieti ya kudumu itapendekeza majina ya watu watakaogombea katika nafasi mbalimbali ili mmoja miongoni mwao katika nafasi mbalimbali za uongozi apate kuchaguliwa na wanachama wa mkoa husika katika mkutano mkuu wa mkoa.

G:SURA YA SABA;VIKAO/MIKUTANO
1)TAIFA
(i)Mkutano mkuu utafanyika mara moja au zaidi kwa mwaka kama itakavyopendekezwa/itishwa na mwenyekiti kwa kushirikiana na sekreterieti ya kudumu kupitia katibu mkuu.
(ii)Vikao vya sekretarieti ya kudumu vitafanyika si chini ya mara mbili kwa mwaka kama itakavyoitishwa na mwenyekiti.
2)MKOA
(i)Mikutano ya wanachama wote wa mkoa itafayika si chini ya mara mbili kwa mwaka.
(ii)Viongozi watafanya vikao visivyopungua vitatu kwa mwaka.

H:SURA YA NANE;UKOMO WA MWANACHAMA/KIONGOZI NA SABABU ZA UKOMO
Mwanachama atafikia ukomo wake wa kuwa mwanachama kutokana na sababu zifuatazo:-
(i)Kutochangia ada kwa mfululizo wa miezi mitatu bila kutoa sababu yoyote ya msingi na kutoonyesha ni lini utalipa deni lako, mwanachama atakuwa amejiengua uanachama mwenyewe.
(ii)Mwanachama atakaposhiriki katika ubadhirifu wowote wa mali za chama.
(iii)Mwanachama kushiriki kwa namna yoyote ile kukisaliti chama ama kujaribu kwa namna yoyote ile kwa makusudi kudhoofisha chama.
(iv)Kiongozi atakuwa amejiondoa uongozi pindi atakapovujisha taarifa zozote za chama.
(v)Pindi kiongozi atakapokiuka maadili ya uongozi na kupoteza imani kwa wanachama kutokana na mwenendo wake usiofaa basi atawajibika kujiuzulu ama kuwajibishwa na srkretarieti ya kudumu baada ya kushauriana na kamati ya nidhamu.
(vi)Mwanachama ama kiongozi atakapotoa taarifa kwa maandishi juu ya uamuzi wake wa kujitoa katika chama ama kiongozi kujitoa uongozi.
(vii)Kutokuhudhuria mikutano/vikao vitatu mfululizo bila sababu ya msingi.
(viii)Kukosa nidhamu kwenye mikutano/vikao na matendo yasiyoendana na mikutano/vikao kama vile kutumia lugha za matusi, kejeli, kutoa tuhuma za uongo, kuleta vurugu nk.
(ix)Kupatikana na uthibitisho wa makosa ya jinai.
ZINGATIO;
Mwanachama atakayejiondoa au kufukuzwa uanachama kwa kutotimiza masharti ya chama ama kutokana na sababu zilizoainishwa hapo juu, hatarudishiwa kiasi chochote cha michango yake.

I:SURA YA TISA;MWISHO
1)KATIBA
Kipengele chochote cha katiba hii kinaweza kubadilishwa wakati wowote wa mkutano mkuu wa chama.